Mkuu mpya wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Maulid Dotto, amekabidhiwa rasmi jukumu la kuendeleza Kampeni ya Tutunzane Mvomero inayolenga kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima pamoja na kuimarisha uchumi wa wananchi waishio kwenye maeneo yanayoathirika na wanyama waharibifu kama vile tembo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika Julai 2, 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya hiyo Mhe. Judith Nguli aliyekuwa Mkuu wa Wilaya amesema kuwa aliipokea Wilaya hiyo ikiwa na changamoto kubwa tatu zikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya ardhi pamoja na wanyama waharibifu.
Aidha, ameongeza kuwa katika kutatua changamoto hizo alibuni Kampeni ya "Tutunzane Mvomero" ambayo imeletea matokeo chanya kwani changamoto hizo kwa kiasi kikubwa zimepungua, hivyo ameikabidhi kampeni hiyo mikononi mwa Mhe. Maulid Dotto ili kuendeleza pale alipoishia.
"...kwa hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya Kampeni hii nakukabidhi nakuomba uendelee hapo nilipoishia mimi inawezekana ukafanya vizuri zaidi kuliko nilivyofanya mimi..." amesema Mhe. Judith Nguli.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Maulid Dotto amemshukuru Mhe. Judith Nguli kwa mapokezi mazuri na miongozo tangu siku ya kwanza ya uteuzi wake huku akiahidi kuwa ataendeleza mazuri ya mtangulizi wake akiwataka watumishi kumpatia ushirikiano ili kuyafikia mafanikio yaliyokusudiwa.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wa Wilaya ya Mvomero Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Dkt. Phillipina Phillipo amesema katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Judith Nguli alisimamia ukusanyaji wa mapato ambapo hadi kufikia Juni 29, 2025 mapato hayo yamefikia asilimia 102. Aidha, amemkaribisha Mhe. Maulid Dotto huku akiahidi ushirikiano ili kuhakikisha kuwa Mvomero inavushwa kwenda mbele.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.