Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikuku (kazi Maalum) Captain Mstaafu Mhe. George Mkuchika (MB) ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inawagusa Wananchi.
Mhe. Mkuchika amesema hayo Oktoba 27, 2024 wakati akizindua mradi wa maji Kata ya Mangae ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya siku moja Wilayani Mvomero ya kukagua, kutembelea na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mhe. Mkuchika ameeleza kuwa nia ya Serikali awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maji hapa nchini ili kumtua mama ndoo kichwani huku akiwapongeza watendaji wa Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri wa fedha na kuweza kutekeleza miradi huo wa maji kwa kiwango cha juu.
"...Naishukuru Halmashauri kwa kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizi hamkuruhusu mchwa kula noti za hapa..." amesema Mhe. George Mkuchika.
Awali, wakati akimkaribisha Waziri Mkuchika, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huo kwa kuwajali na kuwaletea miradi mbalimbali hususan ya maji ambapo hapo awali kipindi cha kiangazi idadi kubwa ya mifugo hufariki kwa sababu ya uhaba wa maji ya kutosha.
Aidha, amesema uwekezaji huo wa tenki la maji katika kijiji cha Mangae utaondoa changamoto ya upatikanaji wa maji huku akitumia fursa hiyo kumuomba Rais Samia kuendelea kutoa fedha ili kuweza kumaliza kabisa adha ya maji.
Naye, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mvomero Mhandisi Mlenge Nasib wakati akisoma taarifa ya mradi huo wa maji amesema mradi huo umegharimu jumla ya shilingi Milioni 643.7, fedha zilizotumika ni shilingi Milioni 388.8 ambapo mradi huo umefikia asilimia 85% kukamilika huku akibainisha kuwa mradi huo utahudumia wakazi 4049 wa kijiji cha Mangae na maeneo jirani.
Nao wakazi wa kijiji hicho akiwemo Bi. Clinsensia Cosmasi amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaletea mradi huo wa maji ambapo hapo awali walikuwa wakichota maji kwenye mito ambayo siyo salama kwa afya zao lakink kupitia mradi wanaamini utakapokamilika utaenda kuondoa adha walizokumbana nazo kutokana na kutafuta maji.
Akiwa Wilayani Mvomero Mhe. Mkuchika ametembelea miradi mitano ya maendeleo ikiwemo ya Afya, Elimu na miundombinu ya Barabara.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.