Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ipo mbioni kutekeleza ujenzi wa Mnara wa Mawasiliano katika Kijiji cha Msolokelo kilichopo Kata ya Pemba Wilayani Mvomero ili kuwaondolea adha wananchi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakipata changamoto hiyo kwa muda mrefu.
Hayo yamebainishwa Disemba 03, mwaka huu na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa akizungumza na wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni ziara ya siku moja ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano Vijijini.
Waziri Silaa amesema kuwa Mnara huo ni miongoni mwa minara 14 inayojengwa Wilayani Mvomero ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata mawasiliano ya uhakika.
"...tumekwisha ongea na Vodacom kwa ajili ya ujenzi wa mnara wa Kijiji hiki cha Msolokelo..." amesema Mhe. Silaa.
Aidha, Waziri huyo amemuagiza Meneja wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Kanda ya Mashariki kushirikiana na Mbunge wa Mvomero Mhe. Jonas Van Zeeland pamoja na Viongozi wengine ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji kuhakiki maeneo mengine ambayo itajengwa minara hiyo 14ya mawasiliano ndani ya Wilaya hiyo.
Katika hatua nyingine Waziri Silaa amewataka wananchi wa kijiji cha Msolokelo na maeneo mengine ambako mradi wa minara 758 inajengwa kuwa wavumilivu na wenyesubira wakati Serikali ikiendelea kufanya kazi na kuhakikisha kuwa nia ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufikisha mawasiliano kwa watanzania inafanikiwa.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mvomero Mhe. Jonas Van Zeeland akieleza changamoto ya mawasiliano katika Kata ya Pemba hususan kijiji cha Msolokelo amesema japokuwa kata hiyo ina mnara mmoja ambapo walitarajia mnara huo ungetatua changamoto ya mawasiliano ya kijiji hicho lakini kutokana na eneo hilo kuzungukwa na milima hivyo kijiji kinahitaji kuwa na mnara wake.
Ameongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia mradi wa minara 758, jimbo la Mvomero limepata minara 14 lakini hadi sasa ni minara sita huku akibainisha kuwa sababu zinazotolewa na wataalam haziridhishi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) Mhandisi Peter Mwasalyanda wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa minara 758 amesema Mkoa wa Morogoro umepata minara 69 yenye thamani ya shilingi bilioni 11.17 ambayo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo. Hadi kufikia Disemba 02, 2024 jumla ya minara 19 tayari imekamilika na kuwashwa.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mhe. Yusuf Makunja amemshukuru Waziri Silaa kwa ziara hiyo yenye matumaini kwa wananchi wa Mvomero hususan katika upatikanaji wa mawasiliano ndani ya Halmashauri hiyo.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.