Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Maulid Dotto, amewahimiza wananchi wa wilaya hiyo kujiunga na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili waweze kupata huduma za afya kwa uhakika na kwa wakati akisema kuwa Serikali imeweka utaratibu rafiki unaomwezesha mwananchi kujiunga kwa gharama ya Shilingi 150,000 kwa mwaka kwa familia ya watu sita.

Mhe. Dotto ametoa wito huo Januari 30, 2026 wakatika akitoa salam za Wilaya kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilicholenga kujadili taarifa za Robo ya Pili (Oktoba Disemba 2025), kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.

Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila kuachwa nyuma, huku akiongeza kuwa viongozi wa ngazi zote wanapaswa kuendelea kutoa elimu ili wananchi wajitokeze kujiunga.



“...mpango huu ni utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha huduma za Afya zinawafikia wananchi wote kwa usawa bila ubaguzi, ambapo kupitia mpango huu kaya italipa kiasi cha shilingi laki moja na elfu hamsini (150,000) kwa mwaka na bima hiyo itawahudumia watu sita kwa familia moja...” amesema Mhe. Dotto.





Aidha, ameongeza kuwa mpango huo ni utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote (Universal Insurance Act of 2023) ambao unalenga kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wakiwemo Wazee, Watoto, Wajawazito na watu wenye ulemavu kupata matibabu kwa gharama zitakazotolewa na Serikali.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mhe. Koila Kurman Majuka amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa salam Pamoja na maelekezo aliyatoa hukua akimuhakikishia kuwa Waheshimiwa Madiwani kwa umoja wao watahamasisha wananchi kujiunga na mpango huo wa Bima ya Afya kwa Wote.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg. Paulo Faty amebainisha kuwa Halmashauri imejipanga kuhakikisha kuwa wananchi waliokusudiwa kujiunga na mpango huo wanajitokeza kwa wingi kwa kutoa hamasa ili lengo la Serikali la kuwapunguzia wananchi mzigo.

Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.