Wanawake wa wilaya ya Mvomero wamehamasishwa kutambua na kuthamini nafasi zao muhimu katika jamii kwa kuwa wana mchango mkubwa katika maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa Machi 5, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli wakati wa maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya Wanawake ambayo kiwilaya yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri yakiwa na kaulimbiu isemayo "Wanawake na Wasichana 2025; Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji".
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Nguli amesema kuwa wanawake wanahitaji kutafakari na kutambua nafasi zao katika jamii kuanzia ngazi ya familia na hata taifa hii itawasaidia kujiamini katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
"...tunatakiwa kujitafakari kama wanawake...sisi wanawake nafasi yetu ni ipi...tukijitafakari tutaona nafasi yetu ni ikowapi..." amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa mwanamke akitambua nafasi yake kwenye jamii na taifa, kunamsaidia kupata fursa sawa na wanawake wengine katika kushiriki shughuli za kiuchumi na Uongozi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Loema Peter amewashukuru na kuwapongeza wanawake wa Wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kuadhimisha siku hiyo huku akibainisha kuwa ni ishara ya kwamba wanawake wanathamini siku hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Mvomero Bi. Recho Kingu amesema kwa sasa jamii imepata uelewa juu ya haki sawa (50 kwa 50) na kwamba wanawake wanapata fursa sawa na wanaume kuanzia kwenye uongozi ambapo idadi ya Wanawake kwenye nafasi za uongozi inaongezeka kila siku.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.