Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika Wilaya ya Mvomero imepongezwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 kwa kutekeleza miradi ya maji kwa ufanisi hivyo, kupunguza adha ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Wilaya hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa Aprili 13, 2025 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 Ndg. Ismail Ali Ussi wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji maji uliopo katika Kata ya Mangae.
Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amesema kuwa katika maeneo ambayo mwenge huo umepita umeshuhudia ufanisi mkubwa uliofanywa na RUWASA katika kutekeleza miradi yake kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Aidha, ameongeza kuwa ufanisi huo unajidhihirisha Wilayani Mvomero ambapo RUWASA imejenga mradi wa maji ambao ni mkombozi kwa wananchi wa Kata ya Mangae.
“...leo hii ndani ya Wilaya ya Mvomero inaonesha jitihada gani ambazo wanazifanya kama wenzetu katika kuwasaidia wananchi hongereni sana wenzetu wa RUWASA...” amesema Ndg. Ismail Ussi.
Sambamba na hilo Kiongozi huyo wa Mbio wa Uhuru amewasisitiza wananchi kutunza miundominu ya maji ili iendelee kudumu kwa muda mrefu na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mvomero Mhe. Jonas Van Zeeland amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwatatulia kero ya maji wananchi wa Mangae ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji safi na salama. Aidha, Mhe. Zeeland amebainisha kuwa miradi ya maji inayotekelezwa katika Wilaya hiyo inagharimu zaidi ya shilingi bilioni 15 huku akiongeza kuwa wahandisi wanaendelea na kazi.
Naye, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mvomero Mhandisi Mlenge Nasibu amesema mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi milioni 643,750,000 chanzo cha fedha ni P4R yaani lipa kwa matokeo. Mhandisi Mlenge
ameongeza kuwa Manufa ya mradi huu ni kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi wapatao 4049.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.