Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Kampeni ya Tutunzane Mvomero leo Agosti 3, 2024 huku akisema kuwa ni ya mfano hapa nchini katika kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Akizungumza wakati akizindua kampeni hiyo Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza viongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwa na mpango madhubuti wenye dhamira ya kudumisha amani kwa kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji ndani ya Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa Ujumla huku akibainisha kuwa mradi huo ni wa mfano kwenye maeneo yote yenye migogoro.
"...Serikali inaunga mkono Kampeni hii ambayo inaweza kuwa ya mfano kote nchini..." amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amebainisha umuhimu wa kampeni hiyo ambapo amesema mradi huo unaenda kuepusha migogoro na kudumisha amani kwenye maeneo husika, kuwezesha ufugaji wa kisasa, kuwawezesha wakulima kuongeza tija ya uzalishaji, mradi utasaidia wakulima na wafugaji kukopesheka kupitia hatimiliki zao pia mradi huo utasaidia utunzaji wa mazingira.
Sambamba na hilo, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuweka msukumo katika kuboresha Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuwa sekta hizo zina fursa nyingi na zimeajiri watu wengi zaidi.
Naye, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa jitihada alizozifanya juu ya kampeni hiyo ambayo imewezesha watu 1066 kujiunga katika kampeni hiyo. Aidha, amebainisha kuwa Serikali imetenga kiasi cha milion 70 kwa ajili ya uchimbaji wa visima 60 Wilayani Mvomero. Ameongeza kuwa Msimu ujao wa Kilimo Wizara italeta tani 50 ambazo zitawasaidia wakulima waishio karibu na hifadhi ya Mikumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru Rais Samia kwa kuzindua kampeni hiyo ya tutunzane ambayo inaenda kuwa chachu ya utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji katika Mkoa huo pia amesema kampeni hiyo itatumika katika wilaya zote ambazo zinachangamoto ya wakulima na wafugaji.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.