Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imeweka mikakati madhubuti ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Hayo yamebainishwa Februari 19, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Loema Peter kwenye kikao cha Baraza la Kata kilicholenga kujadili taarifa za Kata kwa Robo ya Pili kipindi cha mwezi Oktoba - Desemba 2024, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Loema amesema kuwa hatua mbalimbali zitachukuliwa ili kuhakikisha mapato yanaongezeka kwa ufanisi
"...kwenye eneo la mapato tunakwenda kuandaa na timu yangu ya wakuu wa idara pamoja na wengine upande wa mapato tutakwenda kuandaa namna nzuri ya ufuatiliaji wa mapato..." amesema Mkurugenzi.
Aidha, Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuandaa muundo mpya wa namna ya kuandaa taarifa za ukusanyaji wa mapato kwa kila kata, pia amesema kata zitashindanishwa kwenye utekelezaji wa zoezi la kukusanya mapato huku akisema kuwa zawadi zitatolewa kwa kata zitakazo fanya vizuri katika kukusanya mapato.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Mhe. Christopher Maarifa amempongeza Mkurugenzi huyo kwa mikakati hiyo ambayo anaamini itasaidia kuivusha Halmashauri kutoka ilipo sasa, na kuwataka Waheshimiwa Madiwani, watendaji na wataalam wa Halmashauri hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha ili mikakati hiyo iweze kufanikiwa.
Kwa upande wao baadhi ya Waheshimiwa Madiwani akiwemo Mhe. Hamidu Zuberi Diwani wa Kata ya Lubungo alipokuwa wakichangia kuhusu ukusanyaji wa mapato amesema changamoto kubwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara katika kata hiyo hali inayopelekea kushuka kwa mapato.
Aidha, Mhe. Zuberi ameunga mkono hoja ya Mkurugenzi Mtendaji ya kushirikiana na Wakala ya barabara za Vijijini na Mijini - TARURA ili kuboresha miundombinu ya barabara.
Nao Watendaji wa Kata wamewasilisha taarifa za maendeleo ya Kata zao wakilenga zaidi ukusanyaji wa mapato huku changamoto kubwa ikiwa ni miundombinu ya barabara wakisema kuwa miundombinu hiyo ikiboreshwa mapato yataongezeka.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.