Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imekusudia kutumia sheria ndogo kuwachukulia hatua baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wa Sekondari wanaoshindwa kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni, hatua inayolenga kuboresha lishe na kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Hayo yamebainishwa Juni 2, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg. Loema Peter wakati akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Lishe Wilaya ya Mvomero kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa licha ya elimu ya mara kwa mara kutolewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa chakula shuleni, bado kuna baadhi ya wazazi ambao wamekuwa wagumu kuchangia huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya watoto wao. Hivyo, amebainisha kuwa kuna haja ya Halmashauri kutumia sheria ndogo zilizopo ili kuwabana wazazi ili waweze kuchangia chakula cha Watoto wao shuleni.
"…naomba hawa wazazi asilimia 46 kaainisheni watoto wao, halafu wakabidhini kwa watendaji wa Vijiji na Kata wachukue hatua kwa hao wazazi ambao hawataki kutoa chakula shuleni kwa ajili ya Watoto wao wenyewe…tutumie sheria ndogo tuchukue hatua…” amesema Mkururugenzi.
Aidha, Ndg. Loema amesema kuwa utekelezaji wa sheria hizo utaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wazazi ili kuhakikisha wanatambua wajibu wao katika malezi na maendeleo ya watoto wao kupitia mchango wa chakula mashuleni.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kaimu Afisa Elimu Sekondari kutoka halmashauri hiyo, amesema hali ya utoaji wa chakula shuleni kwa shule za sekondari imefikia asilimia 54 huku asilimia 46 ya wanafunzi hawapati huduma hiyo.
Kwa upande wake Afisa Elimu Awali na Msingi wa Halmashauri hiyo amesema shule 160 kati ya 167 wanafunzi wake wanapata chakula shuleni huku shule 7 wanafunzi wanapata uji.
Naye, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Niyonzima wakati akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa viashiria vya lishe kuanzia Julai 2024 hadi Mei 2025, amesema kuwa hali ya utoaji wa chakula shuleni umefikia asilimia 87, kupitia maadhimisho ya siku ya Afya na lishe vijijini Halmashauri imeweza kuwatambua watoto 35 wenye utapiamlo.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.