Mradi wa Sauti Zetu unaotekelezwa na Shirika la SAWA Wanawake Tanzania unalenga kuwakomboa watu wenye ulemavu hususan katika upatikanaji wa haki za msingi ikiwa ni pamoja na elimu, afya, ajira, na ushirikishwaji katika maamuzi ya kijamii.
Hayo yamebainishwa Novemba 26, 2024 na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Dkt. Phillipina Phillipo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa elimu jumuishi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Philippina ameshukuru Shirika la SAWA kwa kuja na mradi huo wa Sauti Zetu ambao unalenga kuvunja vikwazo vya kijamii na kiuchumi vinavyowakumba watu wenye ulemavu kwa kuwapatia fursa na zana za kujisimamia.
Aidha, amesema kumekuwa na changamoto katika jamii kwamba baadhi ya wazazi hawatoi taarifa za uwepo wa watu wenye ulemavu katika familia zao badala yake wanawafungia ndani na kuwanyima haki zao ikiwemo ya kupata elimu na huduma za afya, huku akibainisha kuwa mradi huo utasaidia jamii ya wanamvomero kutoa taarifa za walemavu ili wanufaike na fursa mbalimbali.
“...kwanza nishukuru hili suala wa sababu tunajua ni changamoto ambayo ipo kila sehem...kupitia huu mradi wananchi tutahamasika na tutakuwa tupo tayari kuhusiana na watu wenye ulemavu..." amesema Dkt. Phillipina.
Sambamba na hilo, Dkt. Phillipina amebainisha mipango ya Serikali ambayo inawagusa watu wenye ulemavu ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile vyoo maalum kwa ajili ya wenye ulemavu kwenye shule na vituo vya Afya pamoja na Serikali pia inatoa mikopo ya asilimia 10 ambayo hutolewa na Halmashauri ambapo asilimia 2 ni kwa ajili ya kundi hilo.
Naye, Bw. Mahamud Ngamungi ambaye ni Afisa Ubora wa Elimu kutoka shirika la SAWA Wanawake Tanzania amesema kikao hicho kimewakutanisha wadau wa elimu jumuishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambao walishiriki zoezi la ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi ambao ulianza mwaka 2021 na utaisha mwaka 2026. Ameongeza kuwa mradi wa Sauti Zetu unamaanisha ni sauti za wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo mahitaji hayo yanahitaji kuzingatiwa ili waweze kupata elimu bora.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Msasani Mwl. Immanuel Kahaya amelishukuru Shirika la SAWA kupitia mradi wa Sauti Zetu ambapo mradi huo sio tu kuwapatia elimu bali umechangia kuboresha miundombinu ya wanafunzi wenye ulemavu katika shule hiyo, huku akiishukuru Serikali kwa kutoa fedha za chakula kila mwezi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.