Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mvomero imeagiza mmiliki wa mgodi wa dhahabu uliopo katika Kata ya Doma kukamilisha miundombinu muhimu mgodini ndani ya siku tatu, agizo hilo limetokana na ukaguzi uliofanywa na maafisa wa madini na kugundua mapungufu yanayoweza kuhatarisha usalama wa wafanyakazi na mazingira.
Agizo hilo limetolewa Januari 27, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli alipotembelea mgodini hapo na kujionea hali ya usalama na miundombinu duni inayohatarisha maisha ya wachimbaji na kutoa maelekezo kwa mmiliki wa mgodi huo.
"...sasa leo tutakagua hapa na tutamtaka mwenye eneo hili aweke miundombinu hiyo haraka ndani ya siku tatu tukute hivyo vitu viko tayari...usilale usiku na mchana vinginevyo tutafunga huu mgodi...” amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Nguli amewataka wachimbaji katika mgodi huo kujilinda dhidi ya wanyama wakali kama simba na tembo kwani eneo hilo lipo karibia na hifadhi. Pia, amesisitiza umuhimu wa kulinda mazingira kwa kuhakikisha taka zote zinahifadhiwa vizuri.
Naye, Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Morogoro Bi. Zabibu Napacho amesema mmiliki wa eneo hilo ambalo lina leseni alitoa taarifa kwenye ofisi hiyo kufuatia kuvamiwa na wachimbaji wadogo waliotoka katika maeneo mbalimbali huku akimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutembelea eneo hilo ili kuhakikisha kuwa wachimbaji hao wanafuata sheria za madini.
Kwa upande wake Mhifadhi Wanyamapori Msaidizi Kata ya Doma Simon Ibrahim ametoa wito kwa wachimbaji wa eneo hilo kuchukua tahadhari zaidi juu ya wanyama hatarishi wakiwemo tembo na simba ili waendelee kuwa salama na kuendelea kujitafutia riziki.
Bw. Amini Membe ambaye ni mmiliki wa mgodi huo ameahidi kufanyia kazi maagizo hayo kwa haraka na kuimarisha usalama wa mgodi. Akizungumzia suala la mapato ya kijiji amesema atahakikisha kijiji kinapata mapato yake kama inavyotakiwa.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.