Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Ndg. Paulo Faty amepongeza jitihada zinazotekelezwa kupitia Mradi wa Behavioural Adaption for Water Security and Inclusion (BASIN) uliopo chini ya Shirika la Shahidi wa Maji kwa lengo la kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi huku akisisitiza kuwa ushirikishwaji wa jamii ni nguzo muhimu katika kufanikisha matokeo chanya ya mradi huo.
Ndg. Faty ametoa wito huo Septemba 10, 2025 wakati akifungua Warsha ya mafunzo kwa Viongozi na Wataalam kuhusu taarifa za Tahadhari ya mapema ili kukabiliana na majanga ya hali ya hewa yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Akizungumza katika warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa Shirika la Shahidi wa Maji pamoja na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni wadau muhimu katika Wilaya ya Mvomero, akiongeza kuwa taarifa za tahadhari za mapema zina mchango katika uzalishaji wa mazao ya kilimo pamoja na malisho ya mifugo.
Aidha, amesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuweka mikakati ya kuishirikisha jamii ipasavyo kwa kuwa ndiyo waathirika wa moja kwa moja kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
“...tuweke mikakati mizuri ni namna gani tutashirikisha jamii zetu, waweze kufahamu ni nini cha kufanya ni kilimo gani sahihi kwa mazingira, matumizi bora ya maji...” amesema Ndg. Paulo Faty.
Ameongeza kuwa Halmashauri itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa wadau wanaosimamia mradi huo ili kuhakikisha rasilimali zinazotolewa zinatumika ipasavyo na kila mwananchi ananufaika.
Kwa upande wake Mratibu wa Utafiti kutoka Shirika la Shahidi wa Maji Bw. Vitus Tondelo amesema kuwa Shirika hilo linajikita katika kutafiti, kuibua na kutoa suluhisho kwa changamoto zinazoikumba sekta ya maji. Aidha, amesema Mradi wa BASIN unahakikisha kuwa tabia za mwanadam zinabadilika ili kuleta uhimilivu mabadiliko ya tabianchi katika upatikanaji wa uhakika wa maji. Mradi huo unatekelezwa katika nchi tatu za Tanzania, Malawi na Bukinafaso, kwa Mvomero mradi unatekelezwa Vijiji vya Kambala, Mkindo, Vikenge na Kinda.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.