Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli, amewataka wananchi wanaotaka kununua ardhi kufuata taratibu zote za kisheria ili kuepuka migogoro na hasara zinazoweza kujitokeza.
Mhe. Nguli ameyasema hayo Januari 30, 2025 wakati akifunga mafunzo elekezi kwa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji pamoja na Watendaji wa Vijiji yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari Mzumbe.
Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la malalamiko kuhusu watu kununua ardhi kiholela bila kufuata utaratibu, jambo linalosababisha migogoro ya mara kwa mara huku baadhi ya Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na watendaji wakitajwa kuwa sehemu ya migogoro hiyo.
“…nitoe agizo kwa wananchi wanao nunua ardhi, kwa mihuri ya mwenyekiti, mtendaji na serikali yake haifanyi wao kuwa halali kumiliki ardhi, hiyo ni batiri, taratibu za uchukuaji ardhi zinajulikana…” amesema Mkuu wa Wilaya.
Ameongeza kwa kuwataka wenyeviti hao kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu za kumilikisha ardhi ya kijiji ikiwa ni pamoja na ridhaa ya mkutano mkuu wa kijiji ambao ndiyo wenye mamlaka ya kudhiria mwanchi kupatiwa ardhi.
Pamoja na hayo, Mhe. Nguli amewataka wenyeviti hao kudhibiti migogoro kwenye maeneo yao ikiwemo migogoro ya ardhi na migogoro ya wakulima na wafugaji ili kuhakikisha kuwa Amani na utulivu vinaendelea kudumishwa katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Halamshauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Stephen Mmanywa amesema lengo ni kuhakikisha kuwa wenyeviti hao wanakwenda kutekeleza majukumu yao kwa usahihi huku akitaja mada zilizofundishwa na wawezeshaji ikiwemo, matumizi bora ya ardhi, sheria za mamlaka za serikali za mitaa, fedha na manunuzi. Pia, Bw. Mmanywa ameeleza kuwa matarajio yao baada ya mafunzo hayo ni uwepo wa utawala bora pamoja na kuondoa migogoro ya ardhi na changamoto nyingine za wananchi wa wilaya hiyo.
Naye Bi. Scholastica Nyabweke ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo amewapongeza wenyeviti hao kwa mafunzo hayo huku akiwasisitiza kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya serikali.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Wenyeviti hao, Mhe. Ally Masalika ambaye ni mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiwanjani, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa hotuba nzuri huku akiwashukuru wawezeshaji kwa mada nzuri, pia ametumia fursa hiyo kuwasisita wenyeviti kwenda kuyafanyia kazi mafunzo kwa vitendo katika maeneo yao ili yalete tija.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.