Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Judith Nguli ameonya vikali viongozi wa vijiji na vitongoji wanaojihusisha na uchochezi wa migogoro kati ya wakulima na wafugaji, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na migogoro hiyo.
Mhe. Nguli ametoa onyo hilo Januari 28, mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya utendaji kazi kwa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji pamoja na Watendaji wa Vijiji wa Tarafa za Turiani na Mvomero.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wamekuwa chanzo cha migogoro hiyo kwa kushiriki kugawa ardhi kiholela, kupendelea upande mmoja, au kutoa matamko ya kichochezi huku akibainisha kuwa suala hilo hatolifumbia macho.
“…kwenye suala la migogoro ya wakulima na wafugaji sitokuwa rafiki wa mtu yeyote kwa sababu linaumiza wengi, linatia umaskini wengi…msiturudishe nyuma…” amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Nguli amesema kwa sasa Wilaya hiyo ipo kwenye harakati za kuondoa migogoro hiyo kwa kuwahamasisha wafugaji kupanda malisho na kuchimba visima kwa ajili ya mifugo yao, huku akisema kuwa uhamasishaji huo umeanza kuleta tija ambapo migogoro hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Wilaya amewataka Wenyeviti hao kwa kushirikiana na Watendaji wao wa Vijiji kuhakikisha kuwa wanasoma mapato na matumizi ya vijiji. Pia, amewataka watendaji wa vijiji na wenyeviti kufanya kazi kwa ushirikiano huku wakiepusha migogoro isiyo na tija katika utendaji kwazi wao.
Naye, Katibu Tawala Wilaya hiyo, Bw. Said Nguya amewataka wenyeviti na watendaji hao kuwa na lugha zinazoakisi dhamana waliyokuwa nayo.
Naye Bw. Stephen Mmanywa akimuwakilisha Mkuu wa Idara ya Utumishi na Rasilimali watu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero amesema mafunzo hayo ni ya siku nne ambapo yatahitimishwa Januari 30, 2025, jumla ya wenyeviti wa vijiji 130 na wenyeviti wa vitongoji 687 watapata mafunzo hayo kwa tarafa zote nne.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.