Wahitimu wa Jeshi la Akiba Wilayani Mvomero wamehakikishiwa kupewa kipaumbele katika nafasi mbalimbali za ajira hususan katika vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na vyombo vingine vya usalama kwa kuzingatia sifa na vigezo vitakavyoainishwa na vyombo hivyo.
Ahadi hiyo imetolewa Septemba 12, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Maulid Dotto wakati wa sherehe ya kufunga mafunzo ya Awali ya Jeshi la Akiba, kundi la 10 mwaka 2025 yaliyofanyika katika Kata ya Mtibwa, Tarafa ya Turiani.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali katika ngazi ya Wilaya itaendelea kutoa kipaumbele kwa askari wa jeshi la akiba huku akiwataka kujiendeleza katika fani mbalimbali ili kuongeza sifa za ziada za kuweza kuajiriwa.
"...niwahakikishie kuwa Serikali katika ngazi ya Wilaya itaendelea kutoa kipaumbele kwa wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la akiba katika nafasi za ajira zitakazotangazwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) au vyombo vingine vya ulinzi na usalama..." amesema Mhe. Maulid Dotto.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa makampuni na taasisi za kiserikali kuajiri walinzi waliofuzu mafunzo ya jeshi la akiba ili kuwezesha udhibiti wa matukio na vitendo vya kiarifu ambavyo vinaweza kujitokeza katika maeneo ya makazi au biashara.
Sambamba na hilo, Mhe. Dotto ametoa rai kwa Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya kusimamia na kuhakikisha kuwa wahitimu hao wanapatiwa vyeti vyao pamoja na vitambulisho kwa wakati ili waweze kuvitumia kuomba ajira kwenye taasisi mbalimbali za Serikali na mashirika binafsi.
Kwa upande wake, Mshauri wa Jeshi la akiba Wilaya ya Mvomero Geofrey Mwakabende amesema kuwa mafunzo hayo yalianza rasmi Aprili 28,2025 yakiwa na wanafunzi 65 ambapo idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia wanafunzi 111 huku akibainisha kuwa ongezeko hilo linatokana na uhamasishaji uliofanywa kwa kushirikiana na viongozi wa Kata na Vijiji. Aidha, ametoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi ili waweze kujiunga na mafunzo ya Jeshi hilo la akiba.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.