Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaagiza waajiri wa sekta ya umma na binafsi kuweka mazingira wezeshi ya kuunda vyama vya wafanyakazi na kuacha kudhoofisha vyama vilivyopo katika taasisi zao ili kusaidia kutatua changamoto za wafanyakazi na kupunguza migogoro kazini.
Mhe. Malima ameyasema hayo May 1, 2024 wakati akihutubia Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika Halmashauri ya Mji Ifakara.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kuweka makubaliano ya pamoja ili kuhakikisha vyama hivyo vinawasaidia katika kupata haki zao na maslahi yao kikamilifu.
“...Nitumie fursa hii kwa waajiri wote wa sekta ya umma na sekta binafsi kuwataka kuweka mazingira wezeshi ya kuwepo kwa vyama vya wafanyakazi na kuacha tabia ya kudhoofisha vyama hivyo kwenye taasisi zenu...” amesema Adam Malima.
Aidha Mhe. Malima ameiagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kufuatilia na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kujiridhisha kikamilifu mikataba ya wafanyakazi kama inazingatia sheria na endapo kuna shida ya mikataba ishughulikiwe pamoja na kufanya ukaguzi katika huduma za afya na usalama maeneo ya kazi.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imerejesha utaratibu wa kuwapandisha wafanyakazi madaraja, huku akibainisha kuwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetoa ajira mbadala 26514 pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha ajira 46000, katika kibali hicho ajira za walimu ni 12000 na watumishi wa afya 10000.
Kwa upande wake Mratibu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Morogoro (TUCTA) Bw. Nicholaus Ngowi ameiomba Serikali ifanyie kazi madai ya watumishi ili kuepusha malalamiko yasio ya lazima kwa Wafanyakazi.
Aidha, Bw. Ngowi amebainisha kuwa kero kubwa ya wafanyakazi wa Mkoa wa Morogoro ni mishahara duni ambayo haiendani na gharama za maisha, kucheleweshwa kwa nyongeza ya misharaha kwa wanafanyakazi wanaopanda madaraja, marupurupu yao na kutolipwa posho kwa wakati.
Maadhimisho ya Mei Mosi 2024 yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo "nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao bora na kinga juu ya hali ngumu ya maisha".
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.