Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Ndg. Paulo Faty amesema kuwa matumizi ya mfumo mpya wa ununuzi wa NeST (National e-Procurement System of Tanzania) ukitumika ipasavyo utasaidia kupunguza changamoto za ucheleweshaji wa huduma na upatikanaji wa bidhaa zinazohitajika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali.
Ndg. Faty ameyasema hayo Septemba 18, 2025 wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa NeST kwa watumiaji wa mfumo huo ngazi ya Halmashauri ambayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesisitiza kuwa malalamiko ya ucheleweshaji wa huduma na bidhaa yamekuwa yakileta changamoto katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati huku akisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kufahamu sheria za ununuzi pamoja na usimamizi wa mikataba hivyo, kurahisisha utoaji wa huduma na bidhaa.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa manunuzi hivyo ameruhusu mafunzo hayo kutolewa kwa watumishi wa Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanda ya Pwani kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Bi. Vicky Mollel amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi na watoa huduma ili kuongeza ufanisi katika sekta ya ununuzi wa umma. Ameongeza kuwa mfumo huo unafaida mbalimbali ikiwemo uwazi katika matumizi ya fedha za umma.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi katika Halmashauriya Wilaya ya Mvomero Bi. Aimana Nkya ameishukuru PPRA kwa kutoa mafunzo hayo huku akisema kuwa matumizi ya NeST yataongeza ufanisi na kupunguza changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa manunuzi kupitia mfumo huo.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.