KITENGO CHA UFUGAJI NYUKI
LENGO KUU NA MAJUKUMU YA KITENGO
1.0.UTANGULIZI;
Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kama ilivyo kwa Halmashauri nyingine nchini ilianzisha rasmi kitengo cha Ufugaji nyuki chenye hadhi ya Idara mnamo tarehe 01/03/2014.Kitengo hiki kimeanzishwa kwa mujibu wa waraka namba GA.215/262/01/83 wa Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI uliotolewa tarehe 25/06/2011 kupitia miundo mipya ya Serikali za Mitaa iliyoidhinishwa na Mh.Waziri Mkuu tarehe 08/06/2011.Kitengo kitaendelea kutekeleza shughuli zake kwa kuzingatia Sera ya ufugaji nyuki ya mwaka 1998,Sheria namba 15 ya ufugaji nyuki ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2004.Kimsingi hapo awali kitengo hiki kilikuwa kinawajibika chini ya Idara ya Ardhi na Maliasili mpaka kilipopatiwa hadhi husika na kuweza kujitegemea rasmi huku kikiwajibika moja kwa moja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya husika.
2.0.LENGO KUU LA KITENGO CHA UFUGAJI NYUKI;
Kuongeza mchango wa sekta ya ufugaji nyuki kwa maendeleo endelevu ya ukuaji wa uchumi wa jamii ya Wilaya ya Mvomero na kuboresha uhifadhi na usimamizi wa maliasili zake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
3.0.MAJUKUMU YA KITENGO CHA UFUGAJI NYUKI
3.1.Kuongeza uwezo wa Wilaya kusimamia na kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki kwa kushirikiana na wadau mbali mbali k.m Wakulima,Jumuiya za wananchi(CBOs),Wafugaji nyuki,Sekta binafsi,Serikali kuu,Asasi zisizokuwa za kiserikali na Jumiya za kimataifa pia.
3.2.Kuboresha uhifadhi wa bioanuai,kuongeza ajira na pato la kaya kwa jamii na hatimaye Taifa kutokana na maendeleo ya biashara ya mazao ya nyuki k.m asali,nta n.k
3.3.Kuwezesha kuongezeka kwa ubora na upatikanaji endelevu wa mazao ya nyuki kupitia kilimo mseto ambapo uchavushaji wa maua unaleta ufanisi wa chavua na mbochi.
3.4.Kuhakikisha kuwapo kwa nyuki wa asali kwa kufanya yafuatayo;
i)Kuihimiza jamii kupitia viongozi mbali mbali kujiepusha na uchomaji moto ovyo misitu ili kutunza misitu ambayo ni chimbuko kubwa la maua ya kuzalisha mazao ya nyuki
ii)Kuanzisha hifadhi za nyuki(Bee reserves) zitakazosimamiwa kikamilifu na jamii husika
3.5..Kushiriki katika shughuli za uhifadhi misitu hususani Usimamizi shirikishi wa misitu(kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya misitu(1998),Sheria namba 14 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za mwaka 2004) ili kuwezesha upatikanaji endelevu wa maua kwa ajili ya mbochi(Nectar) na chavua(pollen)
3.6.Kuratibu huduma za ugani wa ufugaji nyuki kadri zinavyohusiana kwa karibu na sekta nyingine k.m wanyamapori,misitu,killimo n.k.
3.7.Kuanzisha,kusimamia na kuendesha hifadhi za nyuki zitakazokuwa zimeanzishwa kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya ufugaji nyuki ya mwaka 1998,Sheria namba 15 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za mwaka 2005 na pia fursa zilizopo k.m.ufadhili n.k
3.8.Kushirikiana na Idara ya maendeleo ya jamii katika shughuli za uhamasishaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usajili wa kisheria wa vikundi na mashirika ya kijamii(CBOs) vinavyojihusisha na ufugaji nyuki unafanikiwa.
3.9.Kushirikiana na sekta ya Ushirika katika kuhakikisha kuwa vikundi vyenye sifa stahiki vinaanzisha ushirika wa kuweka na kukopa(Saccos) wa wafugaji nyuki ili kumudu gharama za uzalishaji mazo ya nyuki na hivyo kuipunguzia Serikali jukumu za kuviwezesha kupitia raslimali fedha,vifaa n.k.
Imetolewa na;
T.D.MWAIKENDA
Mkuu wa Kitengo cha Ufugaji nyuki
Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.